Monday, March 27, 2017

Taifa Stars kuikaribisha Burundi kesho Uwanja wa Taifa

Taifa Stars, Jumanne hii jioni inaingia tena Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kucheza na Intamba Murugamba ya Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, kwa mujibu wa kalenda ya wiki ya mechi za kimataifa ya FIFA.

Huu ni mchezo wa pili kwa Taifa Stars kucheza ndani ya wiki moja baada ya ule wa awali dhidi ya The Zebras ‘Pundamilia’ wa Botswana uliofanyika Uwanja huo wa Taifa, jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
Katika mchezo huo wa Jumamosi, Taifa Stars ambayo kwa sasa inanolewa na Salum Mayanga akisaidiwa na Patrick Mwangata ambao ni makocha wapya wa kikosi hicho, walishinda kwa mabao 2-0.
Tayari Intamba Murugamba wametua nchini tangu jana Jumapili saa 4.30 asubuhi na kufikia Hoteli ya De Mag iliyoko, Kinondoni, Dar es Salaam na jioni yake walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini. Leo Jumatatu, inafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ndani ya kikosi hicho wamo washambuliaji wawili wanaotamba katika klabu za Simba na Young African za Dar es Salaam. Nyota hao ni Amisi Tambwe wa Young Africans na Laudit Mavugo wa Simba.

Leo Jumatatu Machi 27, 2017 saa 8.30 alasiri nyota hao wakiongozana na kocha wao watazungumza na wanahabari namna walivyoajiandaa kucheza na Taifa Stars ambayo pia ina nyota wengi wanaocheza na wachezaji hao wa Burundi katika klabu za Simba na Young Africans.
Wakati Mavugo ni mshambuluaji, anatarajiwa kuwa na wakati mgumu mbele ya walinzi mahiri ambao pia wako Simba kama vile Abdi Banda na Mohammed Hussein wakati Andrew Vicent anayetoka Young African atakuwa kisiki kwa Tambwe wanayecheza naye timu moja kama makocha watawapanga.
Kwa upande wake, Mayanga alifurahishwa na ushindi wa Jumamosi iliyopita dhidi ya The Zebras ya Botswana na hivyo amehimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa kesho.
Katika kuunga mkono wito wa Kocha Mayanga, TFF imebakiza viingilio vya mchezo huo kuwa sawa na vile vya Jumamosi iliyopita kwani katika mzunguko ambao unachukua mashabiki wengi kiingilio kitakuwa ni Sh 3,000.
Kwa upande wa VIP “A” Kiingilio kitakuwa ni Sh 15,000 wakati VIP “B” na VIP “C” kiingilio kitakuwa ni Sh 10,000. Viingilio hivyo vimelenga kuwaalika Watanzania wengine kwenda uwanjani.
Share:

Copyright © TODAY'S YOUTH FOUNDATION | Designed by Francis Ikomba Distributed By Norbert Inc.