Polisi na maafisa wa mamlaka ya mapato nchini Kenya (KRA) leo walifanya jaribio la kuvamia afisi za shirika moja la kutetea haki ambalo lilikuwa limefutiwa usajili Jumanne.
Maafisa hao waliokuwa wamevalia mavazi ya kiraia walifika katika afisi za shirika la Africa Centre for Open Governance (AfriCOG) katika mtaa wa Lavington, Nairobi mapema asubuhi.
Walikuwa kwenye magari wawili wakiwa na agizo walilosema lilitoka kwa mahakama kuwapa idhini ya kufanya uchunguzi katika afizi hizo, wakisema lengo lao lilikuwa kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma za ukwepaji kodi.
Maafisa hao hata hivyo walizuiwa kuingia na viongozi wa mashirika ya kutetea haki za kibinadamu.
Wakili Haron Ndubi amesema walitilia shaka uhalali wa agizo la mahakama ambalo maafisa hao walikuwa nalo.
odi ya kusimamia mashirika yasiyo ya kiserikali ilikuwa imetoa agizo la kutaka shirika hilo lifunge ikisema limekuwa likiendesha shughuli zake kinyume cha sheria.
Mkuu wa bodi ya kusimamia mashirika yasiyo ya kiserikali Fazul Mohammed, pamoja na kufutia usajili shirika hilo, alikuwa amependekeza wakurugenzi wake wakamatwe.
Shirika la AfriCOG liligonga vichwa vya habari mwaka 2013 baada ya kuwasilisha kesi ya kupinga kuchaguliwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi uliokuwa umefanyika mwezi Machi.
Taarifa kwenye vyombo vya habari zimekuwa zikidokeza kwamba huenda shirika hilo linapanga kuwasilisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi ambayo yalitangazwa Ijumaa ambapo Bw Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi.
Hatua ya kufunga shirika hilo ilitangazwa Jumanne siku moja baada ya serikali kufutia usajili shirika jingine la haki za binadamu, Tume ya Haki za Kibinadamu Kenya (KHRC).
Umoja wa Mataifa na shirika la Amnesty International wameshutumu hatua ya kuyafunga mashirika hayo mawili na kuitaka serikali kuruhusu mashirika ya kutetea haki pamoja na wanahabari kuruhusiwa kufanya kazi bila kuhangaishwa.
Mkurugenzi wa Amnesty International katika kanda ya Afrika mashariki Muthoni Wanyeki amesema njia iliyotumiwa na maafisa hao kuvamia afisi za AfriCOG ni kinyume cha sheria.
Amesema ana wasiwasi sana kwamba serikali ya Bw Kenyatta imeanza kuandama mashirika ya kutetea haki za kibinadamu.