Daniel Craig amethibitisha kwamba atarejea kuigiza tena kama James Bond.
Mwigizaji huyo aliulizwa iwapo ataigiza tena kama jasusi huyo maarufu alipokuwa anahojiwa katika kipindi cha The Late Show nchini Marekani.
"Ndio," Daniel alimwambia mtangazaji wa kipindi hicho Stephen Colbert, kabla ya kusimama na kumsalimia kwa mkono.
Mwigizaji huyo, ambaye ameigiza kama 007 katika filamu nne za karibuni zaidi za Bond, alikuwa kufikia sasa amekataa kuthibitisha iwapo angeigiza tena.
Lakini kwenye kipindi hicho cha runinga, alifichua kwamba amekuwa akifahamu hilo "kwa miezi kadha".
"Tumekuwa tukilijadili, tumekuwa tukijaribu kukubaliana jinsi mambo yataenda. Nimekuwa kwa muda mrefu nikitaka kupumzika."
Filamu ijayo ya Bond, ambayo itakuwa ya 25, itatolewa Novemba 2019.
Amesema ataigiza kwa mara ya mwisho kama jasusi huyo maarufu.
"Ninataka kuondoka nikiwa bado navuma, nasubiri kwa hamu sana."
Craig mwenye miaka 49 alikuwa bado anakataa kuthibitisha iwapo ataigiza filamu hiyo ya Novemba hata mapema jana kabla yake kukubali katika kipindi hicho cha runinga.
"Hatujafanya uamuzi wowote," aliambia redio ya Magic 106.7 ya Boston mapema jana.
Craig alichukua nafasi ya Pierce Brosnan kama Bond na filamu yake ya kwanza kuigiza ilikuwa Casino Royale mwaka 2006.
Baada ya hapo, aliigiza katika Quantum of Solace (2008), Skyfall (2012) na Spectre (2015).