Monday, August 14, 2017

Kombora la tani saba lililoibiwa lalipuka kiwandani Urusi

Kombora la kutungua ndege lililokuwa limeibiwa lililipuka na kuwaua watu wawili na kumjeruhi mmoja nchini Urusi.

Kombora hilo la urefu wa mita 10 (futi 35) ambalo liliundwa wakati wa enzi za Usovieti lililipuka likiwa katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa mpya kutoka kwa bidhaa kuukuu mashariki mwa Urusi.
Vyombo vya habari nchini Urusi vilifahamishwa kuhusu mlipuko wa kombora hilo kubwa katika mji wa Chita baada ya video ya mlipuko huo iliyokuwa imepigwa na mtu mmoja akitumia kamera ya gari kuipakia kwenye YouTube.
Kombora hilo ni la aina ya S-200 Angara, ambayo hufahamika kama SA-5 "Gammon" katika mataifa ya Nato.
Makombora hayo yamekuwa yakitumiwa tangu miaka ya 1960 lakini siku hizi nafasi yake imeanza kuchukuliwa na makombora aina ya S-300 na S-400.
Haijabainika ni vipi kombora hilo lilifika katika kiwanda hicho.
Tovuti ya by24.org inasema kwamba kombora hilo la uzani wa tani saba liliibiwa kutoka kwenye kambi ya jeshi na watu wasiojulikana na kuuziwa wakuu wa kiwanda hicho.
Lililipuka wafanyakazi walipokuwa wanajaribu kulibomoa.
Tovuti ya The Insider ilisema wafanyakazi wa dharura walipata kombora jingine aina ya S-200 ambalo halikuwa limebomolewa.
Kisa hicho kimezua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii, wengi wakishangaa ilikuwaje hadi kombora likawa katika kiwanda hicho.
"Tuna silaha nyingi hivi kuukuu nchini Urusi kiasi kwamba watu wanaziuza kama vyuma vikukuu," aliandika mmoja wa watu kwenye mtandao wa VKontakte. Alisema hilo linaweza kusababisha madhara makubwa.
Share:

Copyright © TODAY'S YOUTH FOUNDATION | Designed by Francis Ikomba Distributed By Norbert Inc.