Kiungo wa pembeni wa Mnyama Simba, Shiza Ramadhani Kichuya, ameeleza kuwa, kuna uwezekano wa yeye kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu licha ya kuanza msimu kwa kusuasua tofauti na waliopo juu yake kwa mabao.
Kichuya ambaye alijiunga na Simba msimu uliopita akitokea Mtibwa Sugar, msimu wake wa kwanza akiwa na kikosi hicho alifunga mabao 12 nyuma ya vinara Simon Msuva na Abdulrahman Mussa waliofunga mabao 14.
Kwa sasa Emmanuel Okwi wa Simba ndiye anayeongoza kwenye orodha ya wafungaji katika ligi hiyo akiwa na mabao sita aliyoyafunga baada ya kucheza mechi tatu kati ya nne ambazo timu yake imeshacheza, akiwa na asilimia kubwa ya kuwa mfungaji bora msimu huu, huku Kichuya naye akiwa amepania kumpiku.
Kwa msimu huu, Kichuya kwenye mechi nne alizocheza mpaka sasa, amefunga mabao mawili tofauti na msimu uliopita ambapo kwenye mechi nne za mwanzo alifunga bao moja.
"Naamini bado nina uwezo wa kufunga kutokana na ligi bado ni mbichi sana na pia hao waliotangulia kufunga naamini nitawapita kwa juhudi zangu na hatimaye kuwa mfungaji bora msimu huu," alisema Kichuya.
SOURCE: CHAMPIONI
0 comments:
Post a Comment