Tuesday, September 6, 2016

Kinachowarudisha Nyuma Baadhi Ya Rappers Wa Bongo Ni Hiki

Tanzania imebahatika kuwa na rappers wakali kwa uandishi na wenye uwezo mkubwa wa kutumia kalamu zao kucheza na lugha watakavyo.

Lakini ni rappers wachache tu wanaofaidi matunda ya jasho lao. Ni wachache tu wanaopokea simu kutoka kwa mapromota wanaowaita kwaajili ya show. Ni waimbaji pekee ndiyo wanaoendelea kufaidi na tena inashangaza hata waimbaji wachanga tayari wameingia kwenye orodha ya wasanii walio busy kwa show, pesa kibao zikiwafukuzia.

Lakini kuna kitu ambacho waimbaji wanacho, kinachowasaidia kuwafanya wawe karibu na mashabiki wa kila rika ukilinganisha na wachanaji. Waimbaji wengi wamekuwa na nyimbo zenye ujumbe wa mapenzi ambao hugusa hisia za mashabiki moja kwa moja.
Haimaanishi kuwa rappers nao wanapaswa kuanza kuimba mapenzi pekee kwenye nyimbo zao, bali kuimba vitu vinavyohusisha maisha ya mashabiki. Mapenzi, Matatizo, Stress, Umaskini, Kusalitiwa, Ukosefu wa Ajira, Majaribu, Imani, Maisha ya kila siku, Pesa, Urafiki, Ugomvi, Kula bata, Warembo, ni miongoni mwa mambo yanayowahusu wananchi ambayo kama wimbo ukiyagusa hayo, ni lazima wimbo ufanye vizuri.


Lakini baadhi ya rappers wameendelea kuwa na ujumbe usiokuwa na uhusiano kabisa na mashabiki wao. Kwa mfano, pale ambapo rapper anatunga wimbo kuponda wasanii wa Bongo Flava wanavyobebwa kwenye redio na kupata shows zaidi ama jinsi Babutale anavyosababisha wasanii wengine kukusa mashavu. Jiulize wimbo wenye maudhui kama hayo, msanii ameutunga kwaajili ya nani hasa? Tale ndio ausikie? Ili iweje? Ni promota gani anaweza kukuita ufanye show kwa wimbo wa aina hii?
Wimbo huu una faida gani kwa shabiki ambaye ametoka kwenye kibarua anacholipwa shilingi 3,000 kwa siku na anataka kufungulia redio kusikiliza wimbo utakaozipunguza stress zake? Huoni kuwa akisikiliza wimbo wa Harmonize, Matatizo unaweza kumpa moyo kuwa kumbe si yeye pekee anayesota?

Wimbo huu una mashiko gani kwa kijana maskini aliyegundua kuwa mpenzi wake amemsaliti kwasababu yeye ni maskini na hana fedha ya kumhudumia? Huoni kama akisikiliza wimbo ‘Roho’ wa Fid Q na Christian Bella unaweza kumliwaza? Asikilize wimbo wanaopondwa wale rappers huwaita ‘wabana pua’ ili apate nini kwa mfano?
Wimbo wa kuponda mtu au kundi lililofanikiwa ni ishara ya kukata tamaa! Rappers wengi wanafeli sana kwa kuendekeza harakati za chuki zisizokuwa na tija si tu kwao binafsi, bali hata kwa muziki kwa ujumla. Kama wewe ni bora, jipinde uandike wimbo mkali ukiki! Ama kama wewe ni mkali wa kudiss, kwanini usimdiss rapper wa calibre yako tuone battle itakavyokuwa?
Wakati mwingine unakuta rappers anatoa wimbo unaitwa ‘Noma’ kwa mfano, na ukiusikiliza wimbo huelewi hata amezungumza kitu gani zaidi ya kutaja mada zaidi 100 na kujisifia tu ndani yake! Shabiki atashika nini kwenye wimbo huo? Ni kwasababu wimbo ni kama kitabu au movie, kwamba lazima uwe na ujumbe mmoja unaowakilisha! Lakini wimbo unapozungumza vitu 100 tofauti, ni ngumu shabiki kung’amua kitu, na mbaya zaidi kama wimbo wenye ni mgumu kumeza. Biti ngumu hadi kichwa kinauma unapousikiliza!
Kama rappers wanataka kufanikiwa na kutengeneza nyimbo zitakazokuwa hit, wajifunze kutengeza nyimbo zinazongumzia mambo yanayoendelea katika jamii wanayoihudumia, na si kuimba kile mawazo yao yalipo!
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © TODAY'S YOUTH FOUNDATION | Designed by Francis Ikomba Distributed By Norbert Inc.