Monday, April 10, 2017

SAMATTA KUIBEBA TENA GENK NA KUTINGA NUSU FAINALI LIGI YA EUROPA?


HII ni wiki iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka duniani hasa Watanzania,
ambao shauku yao kubwa ni kumshuhudia mshambuliaji wa Taifa Stars anayecheza klabu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, akikipiga katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Europa dhidi ya Celta Vigo ya Hispania.

Mchezo huo wa kwanza wa robo fainali unatarajiwa kufanyika Alhamisi hii kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Balaidos nchini Hispania.
Samatta ameisaidia timu yake ya Genk kutinga hatua hiyo ya robo fainali baada ya mabao yake mawili kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano, ambao walishinda 5-2 katika Uwanja wa Ghelamco kabla ya mchezo wa marudiano kumalizika kwa sare ya 1-1 wakiwa nyumbani Cristal Arena.
Ushindi huo wa jumla ya mabao 6-3 kwenye mechi mbili za hatua hiyo ya mtoano umeiwezesha Genk, sasa kila Mtanzania atakuwa na shauku kubwa kumshuhudia Samatta akisaka nafasi ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo kama watapata matokeo mazuri katika mechi mbili za robo fainali dhidi ya Celta Vigo.
Samatta aliyeanzia soka lake kwenye klabu ya Mbagala Market, kisha alijiunga Simba na kuuzwa TP Mazembe, ambapo aliichezea misimu minne na kuisaidia klabu hiyo ya DR Congo kunyakua taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 kabla ya kujiunga na Gent.
Nyota huyo alijiunga Januari mwaka jana, lakini hadi sasa hivi ndio kinara wa mabao kwa timu hiyo, ambapo amepachika jumla ya mabao 11 ya Ligi Kuu Ubelgiji (Jupiler League), akifuatiwa na mchezaji mwanzake, Nikolaos Karelis mwenye mabao tisa.
Mabao yake mawili dhidi ya Gent ambayo yameisaidia Genk kutinga robo fainali ndio mabao pekee ambayo amefungwa kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Europa.
Ukiachana na Huruna Moshi ‘Boban’ aliyeikimbia Gefle IF ya Sweden mwaka 2010, Renatus Njohole aliyeichezea Yverdon Sport ya Uswisi kati ya 1999 hadi 2001, Thomas Ulimwengu anayechezea AFC Eskilstuna ya Sweden na nyota wa Deportivo Tenerife, Farid Mussa na wengine wengi, Samatta ndio nyota pekee aliyecheza soka la nje kwa mafanikio akiwa ndiye Mtanzania wa kwanza kushiriki michuano hiyo na kutinga hatua ya robo fainali.
Pamoja na kuwa hii ni robo fainali ya kwanza kwa Samatta, lakini nayo pia ni ya kwanza kwa klabu hiyo ya Gent na bila shaka nyota huyo wa Tanzania atakuwa na kiu kubwa ya kutaka kukisaidia kikosi chake kuweza kutinga hatua ya robo fainali.
Kiu kubwa kwa Watanzania na Samatta mwenyewe ni kuiona klabu hiyo ya Gent ikipangwa na Manchester United, lakini badala yake wakakutanishwa na Celta Vigo, ambayo si timu ya kubeza lakini inaweza ikawa ndio bahati yao kuweza kuitoa na kutinga robo fainali.
Swali ni kwamba Samatta atafanikiwa kuonyesha cheche zake na kuibeba tena Genk kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo?
Share:

Copyright © TODAY'S YOUTH FOUNDATION | Designed by Francis Ikomba Distributed By Norbert Inc.