Monday, April 10, 2017

SIMBA HASIRA ZOTE KWA MBAO, BANDA AFUNGIWA



WEKUNDU wa Msimbazi, Simba, leo wanatarajia  kuendeleza mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, watakaposhuka kwenye dimba la CCM Kirumba, jijini Mwanza
kumenyana na wenyeji wao Mbao FC.

Simba wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na rekodi mbaya ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar uliowafanya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo, huku wapinzani wao Yanga wakiwa wanaongoza ligi.
Tofauti na mechi nyingi, mechi ya leo itakuwa na msisimko  mkubwa kutokana na ukweli kuwa Simba wanataka kupata ushindi kwenye michezo yote iliyosalia, lakini pengine inaweza isiwe kazi rahisi kwao kupata ushindi hasa kutokana na ukweli kwamba Mbao nayo inahitaji kujinasua kwenye mtego wa kushuka daraja.
Mbao imekuwa haina mwenendo mzuri katika siku za hivi karibuni, jambo ambalo linaweza kuwafanya kuingia uwanjani wakiwa na hasira zaidi ya kusaka pointi tatu muhimu zitakazoendelea kuwaweka katika nafasi salama kuepuka kurejea Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha msaidizi Simba, Jackson Manyanja, alisema amepania kufanya vema ili kujiweka kwenye mazingira mazuri hasa katika mbio za ubingwa.
“Kuna watu wameshatutoa kwenye mbio za ubingwa ila nawaambia, kwenye soka lolote linaweza kutokea ndio mana tunapambana kushinda mechi ya leo ili kwanza turejee kileleni mwa msimamo na kurudisha imani kwa mashabiki wetu, lakini pia kuwapa presha wapinzani wetu,” alisema.
Katika hatua hiyo hiyo, mashabiki wa timu hiyo wameona njia pekee iliyobaki kwa sasa ni kuongeza nguvu kwenye kikosi hicho kilichopo Kanda ya Ziwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, matawi mbalimbali yenye nguvu Dar es Salaam yakiongozwa na tawi la Wekundu wa Terminal kupitia katibu wake, Justin Mwakitalima, walisema bado hawajakata tamaa na ubingwa msimu huu kwa kuwa lolote linaweza kutokea.
“Bado hatujakata tamaa kamwe, kama sisi tumeweza kupoteza na Yanga wakakaa kileleni basi hata wao wanaweza kupoteza pia na ndio mana mpaka sasa ubingwa upo rehani, ndio mana tunakwenda Mwanza kuongeza nguvu,” alisema.
Naye Katibu wa tawi la Kimara Kiungule, Kessy Noel, alisema kikubwa kinachotakiwa ndani ya timu hiyo ni umoja ili kuzoa pointi sita kwenye michezo hiyo ya Kanda ya Ziwa kabla ya kurudi Dar es Salaam.
“Kanda ya ziwa tumebakiwa na michezo miwili, hapo kikubwa ni mshikamano na umoja ili kupata pointi sita ambazo zitatusaidia huko mbeleni, kaulimbiu yetu ni ilipo Simba tupo, basi tunaondoka leo kwenda kuongeza nguvu,” alisema.
Tawi la Manzese kwa Mtogole nalo halikuwa nyuma kutoa maoni yao kupitia Katibu wake, Shabani Matola ambaye alisema kuwa timu hiyo inapaswa kurekebisha makosa ya kizembe yalioyotokea kwenye mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar.
“Mtu kama Banda na Juuko siku ile hawakuwa kwenye mchezo kabisa hata Mkude na Mavugo kwa upande wao, kuna haja ya kurekebisha makosa kuelekea kwenye michezo hiyo iliyosalia, pia tunahitaji kuwaombea mabaya Yanga ambao kwa sasa ufunguo wa ubingwa wameushikilia.
“Tupambane na tuongeze nguvu kuanzia wachezaji, viongozi na hata mashabiki tusijisahau kila mmoja afanye kazi yake, naamini kwa Mungu kilio chetu msimu huu atakisikia,” alisema.
Simba mpaka sasa wamebakisha michezo mitano huku wakiwa wamekusanya pointi 55 na kushika nafasi ya pili, huku wapinzani wao Yanga wakiongoza msimamo huo wa ligi kwa kukusanya pointi 56, baada ya kushuka dimbani mara 25.
Share:

Copyright © TODAY'S YOUTH FOUNDATION | Designed by Francis Ikomba Distributed By Norbert Inc.