Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameivunja rasmi Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) na ameagiza mali na
shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na CDA zihamishiwe Halmashauri ya Manispaa
ya Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli
ameivunja CDA kwa kutia saini hati ya Amri ya Rais ya kuivunja Mamlaka hiyo
Ikulu Jijini Dar es Salaam, tukio ambalo limeshuhudiwa na Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Vangimembe Lukuvi, Waziri wa
Sheria na Katiba Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi, Naibu Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Antony Mavunde, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma Bw. Jordan Rugimbana na viongozi mbalimbali wa wizara.
Mhe. Rais Magufuli
amesema ameamua kuivunja CDA na kuhamishia majukumu yake katika Halmashauri ya
Manispaa ya Dodoma ili kuondoa mkanganyiko wa utoaji wa huduma kwa wananchi
uliokuwa ukisababishwa na mgongano kati ya vyombo hivyo viwili na pia kuendana
na mahitaji ya sasa ambayo yamedhihirisha kuwa hakuna haja ya kuwepo kwa CDA.
Kufuatia uamuzi wa
kuivunja CDA, Mhe. Dkt. Magufuli pia ameivunja Bodi ya CDA, aliyekuwa
Mkurugenzi Mkuu wa CDA Mhandisi Paskasi Muragili atapangiwa kazi nyingine na
ameagiza wafanyakazi wote wa Mamlaka hiyo wahamishiwe Halmashauri ya Manispaa
ya Dodoma na ofisi nyingine za Serikali kadiri inavyofaa.
Aidha, Mhe. Rais
Magufuli ameagiza hati zote za kumiliki ardhi zilizokuwa zikitolewa na CDA kwa
ukomo wa umiliki wa miaka 33 zibadilishwe na kufikia ukomo wa umiliki wa miaka
99 kama ilivyo katika maeneo mengine nchini ili kuwavutia wawekezaji hasa wa
viwanda.
“Wananchi wa Dodoma wamelalamikia tatizo hili kwa muda mrefu sana,
hata nilipokuwa kwenye kampeni zangu za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015
walilalamika sana, sasa nimetekeleza niliyowaahidi, naamini kwa uamuzi huu
malalamiko ya wananchi yatapata utatuzi na pia tutakuwa tumeondoa kikwazo cha
umiliki wa muda mfupi wa ardhi uliosababisha wawekezaji kushindwa kujenga
viwanda Dodoma.
“Sasa majukumu yote yanahamishiwa Manispaa ya Dodoma, sitaki
kuendelea kusikia visingizio, mkajipange mambo yaende vizuri” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Makamu wa Rais Mhe.
Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa wamemshukuru
Mhe. Rais Magufuli kwa uamuzi huo na wameahidi kusimamia kwa ukaribu mchakato
wa kuhamisha majukumu ya CDA kwenda Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma.
Mamlaka ya Ustawishaji
Makao Makuu Dodoma (CDA) ilianzishwa kwa Amri ya Rais ya tarehe 01 Aprili, 1973
na kutangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 230 na imevunjwa rasmi leo
tarehe 15 Mei, 2017 kwa Amri ya Rais na kuchapishwa katika gazeti la Serikali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam.