Aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, leo Jumatatu anatarajiwa kuwapeleka mashahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kutoa utetezi wa kesi inayomkabili ya utumiaji wa madawa ya kulevya.
Manji anakabiliwa na kesi hiyo ambayo ilishindwa kusikilizwa Septemba 18, mwaka huu kufuatia wakili wa serikali, Timony Vitalis kumueleza Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha kuwa, kesi hiyo iliitishwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini yeye alidai kuwa alikuwa na safari siku hiyo, hivyo ukianza kutolewa ushahidi atakuwa amechelewa.
Kutokana na wakili wa serikali kueleza hivyo, Hakimu Mkeha alimlaumu Manji kwa kuwa alichelewa kufika mahakamani hapo kabla ya kuomba msamaha huku wakili wake Hajra Mungula akiomba Mahakama iwape kibali cha kupeleka mashahidi wao pamoja na kusikilizwa kwa mfululizo.
Hata hivyo, hakimu Mkeha alikubali maombi yao ya kusikilizwa kesi hiyo mfululizo kwa siku ya leo Jumatatu na kesho Jumanne katika mahakama hiyo.
0 comments:
Post a Comment